Friday 11 March 2016

MTENDE BADO HALI TETE KATIKA LIGI KUU YA ZANZIBAR KANDA YA UNGUJA.



Katika mchezo  uliosukumwa ndani ya dimba la Amani hapa visiwani Zanzibar majira ya saa kumi za jioni, Mtende wamekubali kichapo cha mabao 2-1 walipofungwa na KMKM.

Mabao ya KMKM yamefungwa na Mudrik Muhib katika dakika ya 26, pamoja na Faki Mwalim mnamo dakika ya 45, huku bao la kufutia machozi la Mtende limewekwa kimyani na mchezaji Abbas Nassib katika dakika ya 32.

Katika mtanange huo mlinda mlango wa Mtende Yussuf Salum ametolewa uwanjani baada ya  kuoneshwa kadi nyekundu na mwamuzi Rashid  Farghan mnamo dakika ya 11 kutokana na kumzuia mchezaji wa KMKM Faki Mwalim pale alipokuwa katika harakati za kutaka kufunga bao, na Mtende wakacheza watu kumi katika mchezo huo.

Kocha msaidizi wa timu ya Mtende Kheir Ali Salum amesema kuwa bado wamekuwa wakilalamika juu ya waamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu Zanzibar,
“kitu kinachosababisha matokeo ya timu yetu kuwa mabovu na kutokana na waamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu kwa sababu mpira wa miguu unaendeshwa juu yakanuni na sheria kumi na saba na kanuni zake lakini utakuta uwanjani vitu kama hivyo havitumiki.” Alisema kocha Kheir.

Kwa upande wake kocha Mkuu wa KMKM Ali Bushir Mahmoud,  amesema licha ya kuwa wamepata ushindi lakini vijana wake hawakuweza kucheza kama vile alivyotarajia

“haidhuru tumepata ushindi lakini vijana wangu hawakuwewza kupaform vile nilivotarajia, niweze kusema hawakucheza vizuri hata kidogo kwa mujibu wa maelekezo ambayo nimewapatiza, wanaonekana wanababaika uwanjani hawatulii na mpira wanasahau kila kitu, hii inapelekea kuhatarisha  usalama wa mechi zijazo kwa sababu cheza vizur mechi moja hata kama utapoteza  lakini ucheze vizuri.” Alisema kocha Bushiri.


KMKM sasa wamefikisha alama (27) wakiwa nafasi ya nne (4), na Mtende wao wapo nafasi ya kumi na tatu (13) na wana alama tisa (9).

No comments: