Tuesday 1 March 2016

HASSAN ISIHAKA APIGWA STOP SIMBA.


Kamati ya utendaji ya klabu ya Simba imemsimamisha nahodha wake msaidizi Hassan Isihaka kuichezea klabu hiyo kwa muda usiojulikana baada ya beki huyo kumtolea kocha wake Jackson Mayanja maneno makali kabla ya mechi ya jana ya kombe la FA dhidi ya Singida United.
“Ni kweli tumemsimamisha, amefanya jambo la utovu wa nidhamu kwa kocha wa klabu ya Simba mbele ya wachezaji na viongozi wa Simba jana kabla ya mchezo wetu dhidi ya Singida United”, amesema afisa habari wa klabu hiyo Haji Manara.
“Leo kamati ya utendaji imeamua baada ya kuridhika na maelezo yaliyotolewa na kocha pamoja na yeye mwenyewe (Isihaka) kuzungumza na rais wa klabu. Lazima tulinde nihamu ya wachezaji, kuna ‘codes of conduct’ ambazo zinasimamia maadili ya wachezaji. Tunafahamu kwamba kocha anakuwa ndiye kiongozi mkuu kwenye kambi, mchezaji hawezi kumjibu majibu ambayo si ya kiungwana ukizingatia yeye ni nahodha msaidizi”.
“Jana alikuwa amepangwa kwenye kikosi cha kwanza akasema hawezi kucheza kwasababu hakupangwa kwenye mechi dhidi ya Yanga na anahoji hakuchezeshwa mechi dhidi ya Yanga sasa iweje achezeshwe mechi dhidi ya Singida United”.
“Anahoji vilevile likizo yake ya kukaa benchi imeisha lini mpaka apangwe kwenye mechi ya jana”.
Tangu Simba iwe chini ya Mayanja, kinda huyo wa klabu ya wekundu wa Msimbazi amekuwa hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Dylan Kerr.
(shaffih dauda)

No comments: