Monday 28 March 2016

HAYA NDIYO MAAMUZI YA CAF YALIOFIKIWA BAADA YA CHAD KUKIMBIA KUWANIA KUFUZU FAINALI ZA AFCON,


Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) Jumapili ya March 27 limepokea taarifa kutoka shirikisho la soka la Chad kuhusu kujitoa kwa timu yao ya taifa kwenye mechi za kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Africa (Africa Cup of Nations) zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.
Kwa mujibu wa kifungu cha 61 cha kanuni za mashindano kinasomeka kwamba: “kama timu itajitoa kwenye hatua ya kufuzu kwenye hatua ya makundi, matokeo yake yote yatafutwa (pointi, magoli ya kufunga na magoli ya kufungwa)”.
Kwa maana hiyo, mechi tatu za Chad za kundi G zimefutwa pamoja na matokeo yake kutotambuliwa. Hivyo  msimamo wa undi G utakuwa kama ifuatavyo :
Msimamo wa kundi G kwa sasa unaongozwa na Misri yenye pointi 4, Nigeria pointi 2 na Tanzania pointi 1, timu zote zikiwa zimeshacheza michezo miwili.
Maamuzi ya kamati ya utendaji ya CAF yaliyofanywa January 15, 2015 yalikuwa kwamba, kundi lolote litakalosalia na timu tatu kufuatia kujitoa kwa moja ya timu kwenye kundi hilo, timu itakayoongoza kundi hilo itafuzu moja kwa moja kwenye michuano hiyo.
Kutokana na timu ya Chad kujiondoa kwenye mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Chad limepigwa faini ya dola za kimarekani 20,000 pamoja na kufungiwa kushiriki micuano ijayo ya AFCON kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha kanuni za mashindano ambacho kinaeleza kwamba: “Shirikisho lolote likithibitisha kujiondoa baada ya mechi kuanza kuchezwa litawajibika kulipa faini ya dola za kimarekani 20,000. Pia haita ruhusiwa kushiriki mashindano yanayofuata.
Wakati huohuo, Misri watachuana dhidi ya Nigeria Jumanne  March 29, 2016 Alexandria, Misri.

No comments: