Monday, 7 March 2016

JESHI LA POLISI LAINGILIA KATI KWENYE OFISI ZA ZFA TAIFA KUWAONDOSHA MABAUNSA


Leo ilikuwa ni siku ya makabidhiano baina ya kamati ya Mpito iliokuwa ikiongoza soka la Zanzibar na kamati ya tendaji wa ZFA Taifa ili wakabidhiane Ofisi na nyaraka muhimu za chama hicho.

Lakini zoezi hilo limekwenda ndivyo sivyo na kupelekea mpaka Jeshi la Polisi kuingilia kati katika Ofisi za ZFA Taifa Aman Unguja.

Wakati wajumbe wanakwenda katika ofisi ya chama hicho ndipo walipokuta ofisi hiyo imezungukwa na watu wasiojulikanwa yani ni mabaunsa jambo ambalo limepelekea Kamati tendaji ya ZFA Taifa kuwaita Jeshi la Polisi na kuwashughulikia watu hao.

Punde jeshi la polisi likafika Amani kwenye ofisi za chama hicho majira ya saa 6 mchana na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya watu ambao waliokuwa wakilinda ofisi hiyo , wakati huo huo ndani ya Ofisi hiyo alikuwemo Massoud Attai ambae ni mjumbe kamati tendaji akiwakilisha Wilaya ya Kaskazini “A”,ndipo hapo akatolewa na kuruhusiwa aondoke kwenye ofisi ya chama hicho.

Mussa Suleiman Soraga ambae ni mjumbe wa ZFA Taifa akitokea Wilaya ya Magharibi “A” amezungumza na mtandao huu akisimulia tukio hilo.

“ Kwa masikitiko makubwa tunasikitika, tumekuta walinzi zaidi ya 40, yani mabaunsa wanalinda hapa ZFA, sisi tukaripoti polisi kama ZFA imevamiwa na watu wasiojulikanwa, wakaja polisi wakawakamata na wengine wakakimbia, ofisi ndani alikuwemo Attai akambiwa atoke na Jeshi la Polisi akatuachia ofisi yetu lakini ufunguo katuambia anazo Hussein , ila sisi tumeshanunua kufuli mpya”. Alisema Soraga.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kamati ya Mpito Hussein Ali Ahmada ambapo kamati yake ilitakiwa leo kwenda kukabidhi ofisi na nyaraka za chama hicho amesema yeye hana taarifa kuwa kamati yake ilikuwa inakabidhi ofisi leo hii na wala yeye hana funguo za ofisi za ZFA.


“Kisandu ndo kwanza nakusikia wewe kama leo kulikuwa na makabidhiano kati ya kamati yangu ya mpito na kamati tendaji, sijui jambo hilo, lakini nikuambie Kisandu kamati yangu nilokuwa nikiongoza imekaa kwa amri ya Mahakama, kwa hiyo tupate agizo la Mahakama kuhusu kuondoka kama Mahakama walivotuweka, na kuhusu funguo za ZFA mimi sina kwasababu nikienda ofisini tayari ofisi inakuwa ishafunguliwa”. Alisema Hussein.

No comments: