Mahakama kuu ya Uhispania imeanza kusikiza kesi ya tuhuma za kukwepa kulipa kodi dhidi ya mchezaji nyota duniani Lionel Messi.
Raia huyo wa Argentina na mshambulizi wa klabu bingwa nchini humo Barcelona, anakabiliwa na mashtaka ya udanganyifu na kukwepa kulipa kodi ya takriban dola milioni 4.5 kati ya mwaka wa 2007 na 2009.
Messi na babake Jorge, ambaye ndiye anayesimamia mali yake wanadaiwa kuficha mamilioni ya pesa katika visiwa visivyotoza kodi vya Belize na Uruguay.
Aidha wawili hao wanadaiwa kudanganya maafisa wa kukusanya kodi walipoulizwa awali katika uchunguzi huo.
Mamlaka ya ushuru ya Uhispania inadai kuwa walitumia visiwa hivyo kuficha malipo ya haki miliki ya sura ya mshambulizi huyo matata.
Upande wa mashtaka unataka wahukumiwe kifungo gerezani mbali na kutozwa faini kubwa ili iwe mfano kwa wengine wenye nia kama yao.
Kesi hiyo inatarajiwa kudumu kwa kipindi cha siku 3.
Hata hivyo Messi anatarajiwa mahakamani siku ya Alhamis.
Yeye na Babake wamekanusha madai yote dhidi yao.
No comments:
Post a Comment