Wednesday 8 June 2016

TFF yatuma salamu za rambirambi NFF, CAF na FIFA

Shirikisho la Soka nchini TFF kupitia kwa Rais wake Jamal Emily Malinzi limetuma salamu za rambirambi Shirikisho la Soka Nigeria NFF,CAF pamoja na FIFA kupelekea kifo cha nyota wa zamani wa Nigeria akiwa mchezaji na baadaye kocha Stephen Keshi.

Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, wamepokea kifo cha Keshi kwa masikitiko makubwa kutokana na mchango mkubwa aliokuwa nao katika soka.

Keshi amefariki mapema leo asubuhi ambapo imeripotiwa kuwa alikuwa na maradhi ya shambulio la moyo.

Stephen Okechukwu Keshi alizaliwa Januari 23 mwaka 1962 huko Azare, Bauchi State nchini Nigeria ambapo aliitumikia Nigeria kama beki wa kati kuanzia mwaka 1981 mapaka 1995 na baadaye kuwa kocha wa taifa hilo.

Baada ya muda wake mwingi katika maisha yake ya soka ngazi ya klabu kuutumia akiwa Ubelgiji, Keshi aliamua kwenda nchini Marekani kwa ajili ya mafunzo ya ukocha.

Amewahi kucheza katika timu za Lokeren, Anderlecht, RC Strasbourg, RWDM, CCV Hydra, Sacramento, Scorpions na Perlis FA ambapo maisha yake mengi ngazi ya klabu alicheza klabu ya Anderlecht ya Ubegiji.

Alikuwa kocha wa kwanza mzawa kuipa Nigeria kombe la Afrika na wa pili kutwaa kombe la Afrika akiwa kama kocha na mchezaji pia ambapo kocha wa kwanza kufanya hivyo alikuwa ni Mahmoud El-Gohary wa Misri mwaka 1998.

Aliifundisha timu ya taifa ya vijana ya Nigeria mwaka 2001 katika michuano ya vijana Afrika, vilevile kufuzu kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana mwaka 2001 lakini hata hivyo hakufanikiwa kufuzu.

Baada ya hapo mwaka 2004 mpaka 2006, aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Togo, na kufanikiwa kuipeleka kombe la dunia mwaka 2006 kwa mara ya kwanza kabisa lakini hata hivyo alitimuliwa kabla ya michuano hiyo kuanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani Otto Pfister baada ya Togo kushindwa kufuzu kucheza michuano ya Afrika mwaka 2006 iliyofanyika nchini Misri.
Keshi amewahi pia kuifundisha Mali baada ya kuteuliwa Aprili 2008 kwa mkataba wa miaka miwili hata hivyo alitimuliwa mwaka 2010 baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika hatua ya makundi kuelekea kufuzu michuano ya Afrika.

Keshi aliteuliwa rasmi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Nigeria mwaka 2011 ambapo aliiongoza timu hiyo kufuzu michuano ya Afrika mwaka 2013 na kuchukua taji baada ya kuwafunga Burikina Faso kwa bao 1-0 ambapo punde tu baada ya michuano hiyo Keshi alijiuzulu kutokana na hali ya sintofahamu lakini hata hivyo baadaye walimrejesha.

Aliiongiza tena Nigeria katika Michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2013 ambapo alipata ushindi wa 6-1 dhidi ya Tahiti, akapoteza 2-1 dhidi ya Uruguay kabla ya kufungwa tena na Uhispania mabao 3-0 na kutupwa nje.

Novemba 16 mwaka 2013, Keshi alifanikiwa kuipeleka Nigeria kombe la dunia baada ya kuiondosha Ethiopia kwa wastani wa mabao 4-1 kwenye play-off.

Novemba 18 mwaka 2013, Keshi aliweka rekodi katika soka la Afrika baada ya kuwa kocha pekee wa kiafrika kufanikiwa kuzipekeka timu mbili za Afrika Kombe la Dunia ambazo ni Nigeria na Togo ambapo aliisaidia Nigeria kutwaa ubingwa wa Afrika na kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.

Keshi alifanikiwa kuipeleka Nigeria hatua ya mtoano kwenye Kombe la Dunia mwaka 2014 ambapo walitolewa na Ufaransa baada ya kufungwa mabao 2-0 ambapo katika hatua ya makundi walitoka suluhu dhidi ya Iran, kushinda 1-0 dhidi ya Bosnia na Herzegovina na kufungwa 3-1 dhidi ya Argentina. Baada ya michuano hiyo Keshi alitangaza kujiuzulu.

Baadaye alirudishwa tena na kupewa mkataba mpya ambapo Oktoba 14 mwaka 2014 Keshi alishindwa kabisa kuipa matokeo mazuri Nigeria baada ya kushindwa kupata ushindi hata katika mechi moja kuelekea kufuzu michuano ya Afrika mwaka 2015 ambapo aaada ya matokeo hayo mabovu alitishia kujiuzulu endapo wangeendelea kumpa mashinikizo kutoka kwa watu ambao aliwashutumu kuwa wanamhujumu na baadaye tena alitulia na kusema ataendelea kuifundisha timu hiyo kwasababu analipenda taifa lake.

Keshi aliachana na Nigeria Julai mwaka 2015 baada ya mkataba wake kuisha na waajiri wake NFF kutokuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya na hiyo ilitokana na hali ya sintofahamu iliyokuwa ikiendelea kuwepo kati ya kocha huyo na waajiri wake.

Baada ya hapo Keshi aliamua kupumzika na kufanya shughuli nyingine huku akiwa karibu zaidi na familia yake ambapo Mwaka jana alipata pigo baada ya kufiwa na mkewe ambaye amedumu naye kwa takriban miaka 33 na alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa.

No comments: