Saturday, 18 June 2016

Timu ya Ufaransa inavyoweza kushangaza wengi kama Ujerumani miaka ijayo

Ni wiki moja mpaka sasa tangu ilipoanza michuano ya kombe la Uero inayofanyika huko nchini Ufaransa ikishirikisha timu za taifa 24 kutoka nchi tofauti tofauti kwenye bara la Ulaya.

Michuano hiyo inayoendelea imeweza kuonyesha vipaji vingi ambavyo vilikuwa havipewi nafasi huku baadhi ya timu ndogo zilizokuwa hazipewi nafasi ya kufanya vizuri zikiwashangaza vigogo waliokuwa wanapewa nafasi kubwa kwenye michuano hiyo.

Timu ya Ufaransa ni miongoni mwa timu zinazoshiriki michuano ya Uero kwa mwaka huu iliyokuwa na vijana wengi kwenye mashindano hayo wenye vipaji vikubwa kama Antoine Griezmann, Dimitri Payet, Anthony Martial, Paul Pogba, Kingsley Coman, na wengine wengi, kitu ambacho kimepelekea kutoa nafasi kubwa kwa timu hii kufanya vizuri kwenye mashindano hayo mwaka huu.

Japo hata kama timu hizo zisipofanya vizuri kwenye mashindano hayo kwa mwaka huu pia ipo nafasi ya kuja kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kwa siku za mbele. Miaka kadhaa nyuma timu ya taifa ya Ujerumani ilikuwa haifanyi vizuri kwenye mashindano mengi. Kutokana na hilo, walijaribu kuwekeza kwenye timu yao ya vijana kwa kuwainua baadhi ya mastaa wao wa sasa kama Mesut Ozil, Thomas Mullah, Toni Kroos na wengine wengi.

Baada ya ukame wa vikombe kwa muda mrefu hatimaye mwaka 2014 wakafanikiwa kuchukuwa kombe la dunia lililofanyika nchini Brazil kwa kuifunga timu ya taifa ya Argentina kwa matokeo ya 1-0 kwenye mchezo wa fainali huku goli hilo likifungwa na Mario Gotze, ikiwa na wachezaji wale wale waliowainua takribani miaka 10 iliyopita kutoka kwenye timu yao ya taifa ya vijana.

Hali inaweza ikajirudia kama somo hilo linaweza likatumiwa vizuri na timu ya Ufaransa na Ubelgiji kutokana na kusheheni wachezaji wengi vijana wenye uwezo mkubwa ambao wana muonekano na kuweka historia zilizowahi kuwekwa na wachezaji wakubwa duniani kama Pele, Maradona, Zidane na wengine wengi.

Kwa hilo swali linabaki kwa viongozi wetu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kipi wanaweza kujifunza ili kuinusuru timu yetu ya Taifa Stars iepuke kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu.’

No comments: