Sunday, 27 March 2016

MAJIMAJI WAROA CHAPWAA UWANJANI


Na Is-haq Muhammed.

Ligi daraja la kwanza Taifa Pemba hatua ya 6 Bora imezidi kunoga baada ya timu ya Chuo-Basra kuisambaratisha Maji maji kwa jumla ya mabao 4-0 katika mchezo uliochezwa jana uwanja wa Gombani wakati wa saa 10:00 jioni.

Katika mchezo huo ambao awali ulipangwa kufanyika katika uwanja wa FFU Finya kabla ya kuhamishiwa uwanja huo, ulinzi uliimarishwa ili kudhibiti kile ambacho kilidhaniwa kingetokea kutokana na uhasama uliopo na vurugu kwa kila timu hizo zinapo kutana.

Alikuwa ni Moh`d Salim wa Chuo/Basra aliyeanza kuiandikia timu yake bao la kwanza baada ya walinzi wa timu ya Maji maji simama wakiona kua  ameotea ndipo alipofumua shuti kali lililomshinda golikipa wa Maji maji Abushuri Ali.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko timu ya Chuo/Basra walikuwa mbele kwa bao 1-0, hata hivyo Othman Mussa aliyepoteza nafasi katika dakika ya 8 ya mchezo na Moh`d Said ambaye alikosa nafasi ya wazi katika dakika ya 23, na 44 ambapo wengezitumia ipasavyo hali ingekuwa nyengine.

Kuanza kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kwa timu ya Majimaji kumtoa Said Nassor na kumuingiza Hamad Abdi, huku Chuo/Basra ikiwapumzisha Bakar Shekha na Vuai Maulid na kuwaingiza uwanjani Salum Ali na Saleh Iddi mabadiliko yaliyoonekana kuwanufaisha Chuo/Basra kuliko Maji maji.

Katika dakika ya 51 Vuai Maulid aliipatia timu yake ya Chuo/Basra bao la 2 baada ya kuwazidi ujanja wachezaji wa timu ya Maji maji, na katika dakika ya 65 Salim Ali aliifungia Chuo/Basra bao la tatu na kitabu cha mabao hayo kikihitimishwa  na mfungaji wa bao la kwanza  Moh`d Salim katika dakika ya 86.

Hadi mwisho wa mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Said Ali akisaidiwa na Moh`d Seif na Mwadini Ali Chuo/Basra kutoka Finya FFU 4 na Maji maji kutoka Tumbe walikiwa hawakuambulia kitu.

Hata hivyo mchezo huo ulionekana kuwa na vuta nikuvute,kurupushani  za hapa na pale zilitawala jambo ambalo lilipelekea mwamuzi kutoa kadi mbili nyekundu kwa wachezaji wa timu ya Maji maji na kuwaonya wachezaji kadhaa kutokana na mchezo mchafu.

Waliopewa kadi nyekundu ni Khamis Khatibu na Moh`d Hamad wote wa Maji maji na waliopewa onyo kwa kadi za njano ni Abuu Said, Hamad Bakar, Moh`d Hamad na Khamis Khatibu wa Maji Maji na Vuai Maulid kwa upande wa Chuo/ Basra.


Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa timu ya Chuo/Basra kuvaana na Mkungu Malofa katika uwanja wa Gombani.

No comments: