Njia pekee ya kutosikia ‘maneno ya kejeli na najisifu’ ya Mkuu wa kitengo cha habari wa klabu bingwa nchini, Jerry Muro ni kuzima TV yako mara tu umuonapo akijiandaa kusema, unaweza kuzima radio yako kabla hujaanza kumsikia akizungumza, kuachana na usomaji wa habari gazetini ambayo moja kwa moja ikionyesha kuwa mtu aliyekaririwa humo ni Muro.
Jerry anaisemea Yanga lakini wakati mwingine anatumia kipaji chake kuwafurahisha mashabiki wa timu yake. Yanga ndiyo inayompa kiburi cha kusema, Jerry na wala hasemi vibaya licha ya kwamba nyakati fulani amekuwa ‘akiwakwangua’ wapinzani wao wakuu Simba SC kwa maneno ya ‘dhihaka.’
Wakati Simba inapojaribu kufanya vizuri, Hajji Manara ambaye ni mkuu wa kitengo cha habari klabuni hapo amekuwa akitoa tambo zake, lakini bahati mbaya ni kwamba timu yake haina muendelezo mzuri wa matokeo hivyo anakosa cha kusema zaidi.
Kutishia kumpeleka mahakamani Muro kwa sababu alizotoa Manara ni dalili za ‘mtu aliyeshindwa.’ Iko wapi Simba ile iliyotoa suluhu-tasa na Yanga, Oktoba, 2014? Ile ilikuwa ‘timu ya matarajio ya mbele kwa klabu’, viongozi waliahidi kwamba timu ile ingeendelezwa na kutunzwa zaidi.
Kulikuwa na vijana 6 waliotoka timu ya pili ( Simba B) wakati, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na golikipa, Manyika Peter Jr wakiongezeka na kutengeneza ‘kundi la yosso 8’ ambalo lilipiga mpira mkubwa licha ya mechi kumalizik 0-0.
Manara alitamba sana katika vyombo vya habari, na alitoa kejeli zake kwa Yanga iliyokuwa na mastaa wa bei mbaya, lakini mambo yakaenda hovyo katika mechi saba mfululizo za mwanzo wa msimu, kwani timu yake haikuwa imepata ushindi wowote katika ligi. Angesema nini? Angemtambia nani?
Muro amekuwa akiwabeza wazi Simba kutokana na mafanikio yao madogo ndani ya uwanja katika msimu wa nne. Amefikia kuwapachika jina la ‘WA-MCHANGANI’ na kuiita timu yake ya Yanga ‘WA-KIMATAIFA.’
Kama Manara ataenda mahakani kumshtaki Muro kwa mambo yao ya usemaji katika klabu zao, atashindwa tena na Muro kwani tayari timu yake imechapwa mara mbili mfululizo katika VPL pia, Muro amekuwa mwenye maneno mengi zaidi ya kebehi kumshinda Manara, na huko katika sheria haitaongopa, itamuweka huru Muro.
Manara tayari ameshindwa uwanjani, ameshindwa nje ya uwanja na ataenda kushindwa mahakamani kama atafikia uamuzi wa kwenda huko kwa sababu tu ya maneno ya kebehi ya Muro.
Njia ya kumfunga mdogo Muro ni Simba kuimarisha kiwango chao ili wawe na matokeo bora yasiyoshuka haraka lakini kuendelea kuwa nyuma ya Yanga ni wazi Muro ataendelea kutamba, ataisema kwa vijembe Simba ambayo imekaa juu ya Yanga kwa wiki moja tu katika misimu mitatu sasa ya VPL.
Nilimsikia Manara katika moja ya vituo vya radio akitishia kuwachukulia hatua na kuwapeleka mahakamani wale wote wanao iandika vibaya Simba! Ni dalili ya kushindwa zaidi na wazi mambo yataendelea kuwa magumu upande wake kama timu haitapa matokeo mazuri. Simba SC ni ya nani hasa? Kwanini isichambuliwe? Kwanini isitabiriwe kufanya vibaya?
Simba wanaanza kuweweseka wakati mbaya huu, wakae kimya wasikilize habari na kuzichambua, wamtazame Muro azungumzapo na wajiulize kwa nini anasema sana, wasome makala wanazoona mbaya dhidi yao na wajiulize kwanini wanaandikwa kwa ubaya.
Kutishia kwenda mahakamani bila kujua kosa ulilofanyiwa na mtuhumiwa ni kujipotezea muda. Manara mpeleke Muro mahakamani akapate ushindi mwingine muhimu dhidi yako.
kwahisani ya shffih dauda.
No comments:
Post a Comment