Sunday, 13 March 2016

SIRI KILICHOKWAMISHA AGENDA YA MAREKEBISHO YA KATIBA TFF HII HAPA.

Kikao cha kwanza cha mkutano mkuu wa TFF kimemalizika jana huku story kubwa katika mkutano huo ikiwa ni agenda namba 11 inayohusu mabadiliko ya katiba na wajumbe walikutana kwenye mkutano huo tangu saa nne asubuhi ya jana kujadili agenda mbalimbali.
Kubwa zaidi ni kwamba, wajumbe hao wote kwa pamoja na kwa kauli moja wamekataa kupitisha mabadiliko ya katiba yaliyolenga kupunguza idadi ya wajumbe wa wawakilishi wa mikoa kwa madai kwamba muswada huo haukuletwa kwa muda mwafaka na pia wajumbe hawakupata muda wa kujadili.
Shaffihdauda.co.tz imezungumza na Ally Mayay Tembele mjumbe kutoka mkoa wa Dar es Salaam na mchezaji mkongwe wa klabu ya Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’
“Ajenda za kawaida hazikuwa na shida ingawa bado kuna maeneo mengi yanahitaji marekebisho, agenda ambayo ilikuwa na ukinzani ni ile ya mabadiliko ya katiba ambayo  kwa mujibu wa maelezo ya rais pamoja na kamati ya utendaji ilikuwa ni maelekezo ya FIFA ambayo walipewa wakati ujumbe wa FIFA ulivyokuja mwaka jana 2015”, anasema nyota huyo wa zamani wa soka la Bongo ambaye kwa sasa amejikita katika masuala ya uchambuzi wa soka.
“Lakini kwa hoja za wajumbe wengi, imeonekana ni busara hii agenda ijadiliwe katika mkutano wa mwezi wa 12 mwaka huu kwasababu wajumbe wengi tumekuja kukutana na rasimu ya katiba hapa na inaonesha kuna mikoa wajumbe wamepunguzwa kutoka 13 hadi 7, uwakilishi katika kupiga kura umepungua kutoka kila mkoa watu 4 hadi 1 hayo ni baadi tu ya mapendekezo yaliyopo kwenye katiba mpya”.
“Dunia nzima inaongeza wigo wa kushirikisha watu lakini kwa mtazamo wa katiba hii inaonekana tunabana ushiriki wa wadau wakati kuna tofauti na mabadiliko ya FIFA yaliyofanyika juzi”.
Leo mkutano huo unaendelea ikiwa ni siku yake ya mwisho ambapo mambo mbalimbali yataendelea kujadiliwa. Baada kumalizika kwa mkutano huo, wajumbe watakutana kwa mara nyingine tena kwenye mkutano mkuu mwezi December mwaka huu.

No comments: