Timu ya Strong fire jana imekubali kichapo cha mabao 2-1
walipocheza na Mundu katika mchezo wa ligi daraja la kwanza taifa kanda ya
Unguja hatua ya sita bora.
Mchezo huo uliovurumishwa ndani ya dimba la Amani mjini
Unguja majira ya saa kumi za jioni, Strong fire walikuwa ndio wa mwanzo kuliona
lango la wenzao baada ya mchezaji Ulimwengu Edi Mungi kufunga bao katika dakika
ya 7, lakini ndani ya dakika tatu Mundu wakalipiza mapigo hayo pale Kubo Seif aliposawazisha
katika dakika ya 10.
Katika mtanange huo timu hizo zilionesha upinzani wa hali ya
juu lakini hadi wanakwenda mapumziko zilikuwa sare ya bao 1-1.
Timu hizo ziliporudi kumaliza ngwe ya lala salama zilicheza
kwa kila timu kusaka bao la ushindi na ndipo Moh’d Seif Mangi alipoipatia Mundu
bao la pili mnamo dakika ya 53 ya mchezo huo.
Na mtanange huo ulimalizika kwa Mundu kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Matokeo hayo yanaifanya timu ya Mundu kufikisha alama nne 4
wakiongoza hatua hiyo, na Strong fire kuwa na alama moja baada ya kutoka sare
katika mchezo wake wa kwanza.
Ligi hiyo itaendelea tena leo majira ya saa kumi za jioni
ndani ya uwanja wa Amani kwa kuchezwa mchezo kati ya Wakombozi wa ng’ambo Taifa
ya Jang’ombe kwa kupepetana na timu ya
Chwaka, katika mtanange huo Taifa ya Jang’ombe wataingia uwanjani wakiwa na
alama tatu 3, huku Chwaka wao wataingia wakiwa na alama moja.
No comments:
Post a Comment