Tanzania itaendelea kusubiri hadi mwaka 2019 kucheza fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya hesabu zake za kuishinda Misri kwa mabao mengi kugoma na kuyeyuka kabisa kwa kipigo cha mabao 2-0 nyumbani.
Huku mashabiki wachache wa Misri waliojitokeza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakibeba bango lenye kaulimbiu hiyo maarufu ya Rais John Magufuli ‘Hapa Kazi Tu’, waliitumia kuishangilia timu yao kila ilipoandika bao kupitia kwa mshambuliaji wao hatari aliyewahi kuichezea Chelsea ya England, Mohamed Salah, moja kila kipindi.
Ushindi huo umeirejesha kwenye ramani ya soka nchi ya Misri ambayo leo itafikisha miaka 41 kamili tangu icheze kwa mara ya kwanza dhidi ya Tanzania na kuambulia sare ya bao 1-1.
Timu hiyo, maarufu Mafarao imekuwa ya kwanza barani Afrika kufuzu kwa fainali zijazo zitakazofanyika Gabon mwakani, ikiwa na pointi 10 na kuziacha Tanzania na Nigeria zikisubiri Septemba 3 ili kucheza kwa kutimiza wajibu.
Misri, imecheza mechi 11 dhidi ya Tanzania ikiwamo mechi ya jana, imeshinda mara kumi na kupachika mabao 40, dhidi ya kumi ya Tanzania.
Hata hivyo, kama wasemavyo waswahili, sikio la kufa halisikii dawa baada ya nahodha Mbwana Samatta kupoteza nafasi adhimu kuandika bao kwa mkwaju wa penalti uliopaa, dakika ya 53 ya mchezo huo.
Penalti hiyo ilitokana na Amri Warda aliyeingia kipindi cha pili kumuangusha kiungo Himid Mao katika eneo la hatari.
Salah anayeichezea klabu ya AS Roma ya Italia alifunga bao la kwanza, dakika ya 43 kwa mpira wa adhabu ndogo iliyokwenda moja kwa moja wavuni baada ya beki Haji Mwinyi kumfanyia madhambi Mohamed Elneny, kiungo wa Arsenal ya England, nje kidogo ya 18.
Kuingia kwa bao hilo kulisababisha mashabiki wachache wa Misri kushangilia kwa nguvu huku wakitumia bango hilo la ‘Hapa Kazi Tu’.
Salah aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Taifa Stars ambayo sasa watasubiri kwa miaka 38 kucheza Afcon, aliipatia timu yake bao la pili kwa shuti kali baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania waliozubaa kuokoa mpira.
Misri iliyohitaji sare ya aina yoyote katika mchezo huo wa jana ilipata ushindi huo ambao ni faraja kubwa kwao baada ya kukosa fainali hizo kubwa Afrika tangu mwaka 2010. Mafarao hao wamefuzu moja kwa moja wakiwa na pointi 10 kutoka kundi G.
Katika mchezo huo wa jana,Taifa Stars ilionekana kukamatwa zaidi katika eneo la kiungo kutokana na Misri ikiongozwa na kiungo wa Arsenal Mohamed Elneny kutawala kwa muda mrefu wa mchezo, Kocha Charles Mkwasa alishindwa kusoma vyema wapinzani wake.
Kocha huyo alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Elius Maguli, Haji Mwinyi na Thomas Ulimwengu na nafasi zao kuchukuliwa nao, John Bocco,Mohamed Hussein na Deus Kaseke, mabailiko ambayo hayakuisaidia chochote timu hiyo.
Awali, Stars ilianza mchezo kwa kasi na matumaini makubwa na katika dakika ya 19, Samatta alikosa bao baada ya beki wa Misri Ahmed Hegazy kuokoa mpira huo.
Dakika ya 28, Krosi ya Himid Mao ilitua kichwani mwa Thomas Ulimwengu ambaye hata hivyo alipiga kichwa kilichookolewa kistadi na kipa wa Misri, Essam El-Hadary. Nusura Samatta awainue vitini Watanzania dakika ya 30 baada ya kuachia shuti kali, lakini beki wa Misri aliokoa na kuwa kona tasa.
No comments:
Post a Comment