Mkutano mkuu wa dharura wa Chama cha Mpira wa miguu Zanzibar unatarajiwa kufanyika kesho kwenye ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo uliopo Kikwajuni mjini Unguja.
Miongoni mwa ajenda zinazoenda kujadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na mwenendo wa Kamati Tendaji ya ZFA hiyo kama ilivyokubaliwa kwenye maamzimio ya kikao cha pande mbili na kusajiliwa Mahkama kuu ya mjini Vuga, Zanzibar.
Ajenda nyengine ni kuteuliwa Mkaguzi wa Mahesabu yaani 'Auditors' kwa ajili ya kuvipitia vitabu vya mahesabu vya Chama hicho.
Mbali na ajenda hizo pia ipo ile ambayo itahuisha soka la Zanzibar kwa vizazi vya sasa na vijavyo yaani kuandika upya katiba ya ZFA inayoendana na zile za FIFA, CAF, CECAFA na hata TFF.
Katika kipengele hicho jumla ya wanamichezo kumi na mbili wataingia kwenye mchakato wa kutafuta riadhaa ya wajumbe wa mkutano mkuu huo ili kupewa jukumu la kuiyandika katiba hiyo.
Majina ambayo yataingia katika mchakato huo ni Eliud Peter Mvella (Msaidizi mkurugenzi TFF na Mwanasheria), Saleh A. Said (Wakili upande wa ZFA), Ame Abdalla Dunia (Mwalimu/Taaluma ya Sheria), Omar Makungu (Mwanasheria, Kiongozi na mchezaji wa mpira), Othman Ali Hamad (Mwanasheria, Kiongozi na mchezaji wa mpira), na Mwinyimvua Abdi Mzukwi(Mwanasheria, Kiongozi na mchezaji wa mpira).
Wengine ni Hafidh Ali Twahir (Mkufunzi wa waamuzi na mzoefu wa michezo), Abdalla Juma Mohammed (Mwanasheria), Affan Othman Juma (Kiongozi wa mpira na taaluma ya sheria), Ali Ame Issa (Kiongozi na mchezaji wa mpira), Suleiman Mahmoud Jabir (Mtaalam wa michezo na mkufunzi wa mpira) na Salum Bausi (Kocha na mchezaji wa mpira).
Idadi ya wajumbe watakaopewa jukumu la kuunda kamati hiyo ya kutengeneza katiba mpya ya ZFA itajulikana hapo kesho kupitia mkutano huo.
Mkutano huo utakuwa chini ya Mwenyekiti wake rais wa ZFA, Ravia Idarous Faina kama ambavyo Mahkama kuu imeagiza kupitia makubaliano hayo.
No comments:
Post a Comment