Wednesday 9 March 2016

MIRAJ ADAM: MLINZI ALIYEJIBEBESHA MAJUKUMU YA UFUNGAJI COASTAL UNION

Mlinzi wa pembeni kijana, Miraj Adam tayari ameichezea Coastal Union ya Tanga mechi 11 tangu aliposajiliwa kwa usajili wa mkopo kutoka Simba SC katika dirisha dogo la usajili mwezi Disemba mwaka uliopita.
Mchezaji huyo zao la timu B ya Simba alishindwa kufanya vizuri katika timu yake hiyo kutokana na majeraha ya mara kwa mara tangu alipopandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2012/13. Miraji amefunga magoli manne na ku-asissts magoli mawili huku magoli yake ya freekick dhidi ya Yanga SC na Azam FC yakichangia ushindi muhimu wakati Coastal ilipowaangusha wababe hao wa ligi.
Licha ya kuendelea kufanya vizuri tangu aliposajiliwa klabuni hapo lakini bado timu yake iko mkiani kabisa mwa msimamo ikiwa na pointi 16 tu baada ya kucheza michezo 21. Coastal itacheza na ndugu zao wa Tanga, JKT Mgambo leo Jumatano na ushindi unaweza kuwaondoa chini na kuwapandisha juu kidogo kutokana na tofauti ndogo ya pointi iliyopo kati ya timu 4 za chini.
“Tumejiandaa vizuri na mchezo wetu wa Jumatano, Mgambo ni timu nzuri na wote tunakutana tukiwa katika nafasi mbaya katika msimamo.” Anasema Ally Jangalu kocha wa Coastal ambayo imefanikiwa kufunga magoli 13 tu hadi sasa huku Miraj akiwa ndiye kinara wa ufungaji.
“Tunafanya kila jitahada kuhakikisha tunafunga magoli ya kutosha, nafurahi kuona Miraj akifunga lakini hili ni jukumu la timu nzima. Kama hatufungi si rahisi kushinda mechi hivyo tunajitahidi sisi kama walimu kuhakikisha timu inafunga.”
(shaffih Dauda)

No comments: