Na Is-haq Muhammed Salma Sport's media
Timu ya Chipukizi imeianza vyema ligi kuu ya Zanzibar baada
ya leo kuinyuka wakongwe wenzao wa soka kisiwani Pemba na Zanzibar kwa ujumla
timu ya Jamhuri kwa bao 1-0.
Alikuwa ni mchezaji wa zamani wa timu ya Simba ya jijini
Dar-es salaam Soud Abdalla aliyezitikisha nyavu za Jamhuri jua ikiwa limeshazama katika dakika ya 84.
Katika mchezo ambao ulikuwa wa ushindani mkubwa timu ya
Chipukizi ilionekana kulielemea zaidi lango la Jamhuri hasa katika kipindi cha
kwanza na kama wachezaji Faki Khamis na Rashid Moh`d wangalikuwa makini
wengepeleka madhara mapema langoni mwa wapinzani wao.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakukuwa na
timu iliyoweza kulifuma lango la mwenzake.
Hata hivyo Jamhuri haitaacha kuwalaumu washambuliaji wake
akiwemo Abdalla Othman kutokana na kushindwa kuzitumia nafasi chache
walizozipata katika dakika za 57, 67 na 81.
Akizungumzia SALMA SPORT’S MEDIA juu ya kupoteza
mchezo huo kocha wa Jamhuri Ameir Chua
amesema ni makosa yaliyofanywa na walinzi wake ndiyo yaliyotoa nafasi kwa
wapinzani wao kuwafunga bao hilo, huku akiahidi kufanya vyema katika michezo
ijayo.
Kocha Mzee Ali Abdalla wa Chipukizi amesema mchezo ulikuwa
mkali sana, hata hivyo amesema juhudi zilizofanywa na wachezaji wake zimeweza
kuivusha timu hiyo katika mchezo huo kwa kupata alama 3 muhimu.
Aidha Mzee amesema timu ya Jamhuri sio ya kubeza kutokana na
kiwango kikubwa walichokionyesha katika mchezo huo.
Katika mchezo mwengine wa ligi kuu ya Zanzibari kanda ya
Pemba uliochezwa leo kwenye uwanja wa FFU Finya timu ya Kizimbani imeiadhibu
vibaya timu ya Aljazira kwa kuipiga mabao 4-2.
Timu ya Young Islanders nayo ikaondoka patupu kwa kupokea
kipigo cha magoli 2-1 kutoka kwa African Kivumbi katika mchezo uliochezwa
kwenye uwanja wa Kangani Skuli.
Ligi kuu ya Zanzibar Kanda ya Pemba itaendelea tena kesho kwa
timu ya Dogo Moro kuwaakaribisha Mwenge katika uwanja wa Gombani, ambapo huko
FFU Finya Okapi wataikaaribisha Madungu.
No comments:
Post a Comment