Friday, 1 April 2016

JKU WAZIDI KUJIWEKA KILELENI HUKU POLISI WAKIWA KATIKA WAKATI MGUMU.NA PEMBA NAKO KAMA KAWA.


Timu ya kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) imeendelea kufanya vyema na kuzidi kuiweka kileleni katika michezo yake ya ligi kuu ya Zanzibar kanda ya Unguja baada ya leo kuwabamiza timu ya kikosi cha Polisi mabao 2-0.

Katika mchezo huo uliosukumwa ndani ya dimba la Amani mjjini Unguja majira ya saa kumi za jioni, JKU walianza kupata bao la mapema katika dakika ya kwanza baada ya mchezaji  Emmanuel Martin wa JKU kupiga kross na ndipo mchezaji wa Polisi Mohammed Haji kuifunga wakati alipokuwa katika harakati za kuuokoa mpira huo na ndipo alipowapatia JKU bao la kuongoza.

Mtanange huo uliendelea na ilipofika dakika ya 80 kijana Feisal Salum akaipatia  JKU bao la pili, na mchezo huo ulimalizika kwa JKU kuibuka na ushindi wa mabao  2-0.

Kwa matokeo hayo timu ya JKU imezidi kujiweka kileleni wakiwa na alama 35, huku Polisi wakiwa wanaburuta mkia na alama nane 8.

Wakati huo nako huko kisiwani Pemba ligi kuu imeanza rasmi.

Ikiwa ligi kuu ya Zanzibar kanda ya Ungua ikielekea ukingoni leo ligi hiyo kwa kanda ya Pemba ndio kwanza imeanza rasmi leo hii kwa kusukumwa michezo mitatu katika viwanja tofauti.

Katika michezo hiyo ndani ya dimba la Gombani, Chipukizi wamewafunga  Jamhuri bao  1-0, katika uwanja wa Finya, Kizimbani wamewabamiza  Aljazira  mabao 4-2, na kule katika uwanja wa Kangani, Afrika Kivumbi wamekubali kufungwa mabao 2-1 kutoka kwa Yanga Islander.

No comments: