Friday, 1 April 2016

MASHABIKI WATOKOMEA VICHOCHORONI KWA KUHOFIA KIPIGO UWANJANI.



Kipigo walichokipata timu ya Chuo/Basra inayoundwa na askari polisi  katika dakika za mwisho za mchezo kutoka kwa Danger Boys ya Kangani kiliwapa hasira na kuamua kuwavamia waamuzi na waandishi wa habari na kuwashambulia.

Mara baada ya kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Hassan Gerei kupulizwa washabiki wa timu ya Chuo/Basra ambao karibu ya wote ni askari polisi waliotegemewa kutuliza amani panapotokea vurugu ndiyo waliovamia uwanjani na kuwanza kuwapa kibano waamuzi.


Waamuzi waliopewa kipano hicho kutoka kwa walinda usalama hao ni aliyekuwa mwamuzi wa kati Hassan Abdalla Rashid “Gerei” Msaidizi wake nambari moja Juma Abdalla na Msaidizi namba 2 Moh`d Seif.

Haikujuulikana ni kipi hasa ambacho kilitokea hadi mashabiki hao kuamua kuwashambulia waamuzi baada ya kumaliza kwa mchezo, huku baadhi ya mashabiki waliouona mchezo huo wamedai Chuo/Basra wanapaswa wajilaumu wenyewe.

Pia askari hao walimshika na kumweka chini ya ulinzi na kumpokonya kamera mwandishi wa Habari na Mpiga picha wa Gazeti la Zanzibar Leo  Abdi Suleiman ambaye alikuwepo uwanjani hapo aliopokuwa akijaribu kupiga picha za matukio hayo.

Baada ya kuishikilia kamera hiyo kwa muda na kumweka chini ya ulinzi kwa muda askari hao walimrejeshea kamera yake lakini picha za matukio ya kuvamiwa na kupigwa kwa waamuzi zilikuwa zimeshafufutwa.

Tafrani hizo ziliwafanya baadhi ya watu waliofika kuangalia mpira kutokomea kila mmoja kichochoro chake huku wengine wakidhani kungepigwa mabomu ya machozi.


No comments: