Bao la dakika ya 89 la mchezaji Chedy
Francis wa Dangers Boys ndilo lililoinyima timu ya Chuo/Basra kupata nafasi ya
kucheza ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao, baada ya kujikuta wakichapwa mabao 4-3
katika mchezo wa ligi Daraja la kwanza Taifa Pemba uliochezwa uwanja wa
Gombani.
Timu ya Basra iliyokuwa ikihitaji
kupata sare ya aina yeyote ile katika mchezo huo walijikuta wakinyong`onyewa na
miguu baada ya kuingia bao hilo ambapo hadi katika dakika ya 85 walikuwa
wakiongoza kwa magoli 3-2.
Kiujumla mchezo mzima ulikuwa wa vuta
nikuvute tangu pale mwamuzi Hassan Abdalla Gerei ilipopuliza kipenga cha
kuashiria kuanza kwa mchezo huo, uliochukua kiasi sekunde 10 tu kwa timu ya
Danger Boys kujipatia bao la kwanza lilifungwa na mchezaji wake Chedy Francis.
Bao hilo unaweza kusema kama halikuwatia
simanzi wachezaji na mashabiki wa Chuo/Basra kwani walijipanga kuanza kusukuma
mashambulizi ya kulikomboa goli hilo, na ndipo katika dakika ya 31 Moh`d Salim
alipoisawazishia timu yake bao hilo.
Dakika 6 baadaye yaani dakika ya 37
Chum Ali Haji aliweza kuiandikia timu yake ya Chuo/Basra bao la pili baada
kuusindikiza wavuni mpira akipokea pasi safi kutoka kwa winga wa kulia wa timu
hiyo Juma Chuma.
Hata hivyo kabla ya mashabiki wa
Chuo/Basra hawajakaa chini vizuri baada ya kushangilia bao hilo, Chedy Francis
wa aliisawazishia timu yake ya Danger Boys bao la pili, lakini Mkwaju
uliotokana na adhabu uliopigwa kwa ustadi na Vuai Maulid katika dakika ya 42
uliwapeleka mapumziko Chuo/Basra wakiwa na mabao 3 dhidi ya 2 ya Danger Boys.
Ikiwa mashabiki waliowengi waliofika
uwanjani hapo kushughudia mchezo huo wakidhani kuwa tayari Basra imeshaondoka
na ushindi wa alama 3 uwanjani hapo na kushika nafasi ya pili mchezaji Makame
Sharrif Hamdu aliweza kuisawazishia timu yake ya Danger Boys goli la 3 na
kuzusha shangwe kubwa kwa mashabiki waliokuwepo uwanjani.
Shangwe na kitimtim zilizuka baada ya
Chedy Francis kuifungia timu yake ya Dangers Boys bao la 3 katika dakika ya 89,
na hadi mchezo huo unamalizika Danger Boys 4 Chuo/Basra 3.
Katika mchezo mwengine wa ligi hiyo
uliochezwa kwenye uwanja wa Ngerengere baina ya timu ya Wawi Star na New Star,
timu ya New iliibuka na ushindi wa magoli 4-0.
Kwa matokeo hayo timu ya Danger
waliofikisha alama 7 wanaungana na Wawi Star waliofikisha alama 10 na New Star
waliofikisha Alama 7 kupanda daraja na kucheza ligi kuu msimu ujao.
Wakati huo huo ligi kuu ya Zanzibar
kanda ya Pemba inatarajiwa kuanza leo katika viwanja vitatu ambapo katika
uwanja wa Finya FFU Aljazira watakuwa na Kizimbani, Yong Islanders watasafiri
hadi Kangani kuvaana na African Kivumbi.
Huku macho na masikio yote
yakielekezwa kwa wakongwe wanaotamba katika soka hapa kisiwani Pemba timu ya
Jamhuri ya Wete watakapo oneshana cheche na wagongwe wenzao wa Chipukizi ya
Chake Chake kwenye uwanja wa Gombani.
No comments:
Post a Comment