Thursday, 5 May 2016

MAFUNZO WAICHARAZA KVZ 2-1.


Timu ya Mafunzo imezidi kujiweka katika nafasi nzuri na kujipa matumaini ya kuweza kulitetea taji lao baada ya kuwafunga Timu ya Kikosi cha Valantia Zanzibar KVZ mabao 2-1, katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar kanda ya Unguja.

Mchezo huo uliosukumwa ndani ya uwanja wa Amani mjini Unguja, KVZ  walikuwa ndio wa mwanzo kupata bao lililowekwa kimyani na mchezaji Suleiman Hassan Kede katika dakika ya nane 8.

Mafunzo wakasawazisha mnamo dakika ya 30, kupitia mchezaji Sadik Habib, na mnamo dakika ya 41 Sadik akarudi tena nyavuni kwa kuipatia Mafunzo bao la pili, na mabao hayo yalidumu hadi kumalizika kwa mtanange huo kwa Mafunzo kuondoka na alama tatu kwa ushindi wa mabao 2-1.

Katika mchezo huo Mafunzo walicheza vyema katika kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili KVZ walicheza vizuri kwa kuutawala mchezo lakini walimaliza bila ya mafanikio yoyote kwa kushindwa kuingiza bao katika kipindi hicho cha pili.

Baada ya mchezo huo Mafunzo wamefikisha alama 32 wakiwa nafasi ya nne 4, na KVZ wapo nafasi ya pili na alama 33.

 

No comments: