Klabu ya Arsenal ya Uingereza itashuka ugani Nou Camp kwa
mechi ya marudiano dhidi ya miamba wa Ulaya Barcelona, wakikabiliwa na kibarua
kigumu katika juhudi za kutaka kufika robofainali.
The Gunners wako nyuma 2-0 baada ya kushindwa mechi ya mkondo
wa kwanza nyumbani Emirates.
Meneja wao Arsene Wenger amesema wachezaji wake wamejiandaa
kucheza vyema na kwamba ni muhimu sana kwao kufunga.
“Hatuhitajiki kufanya hesabu sana, tunajua ni lazima
tushambulie na tufunge,” amesema Wenger.
“Wachezaji wameungana pamoja tayari kucheza vyema.”
Arsenal wanahitaji kufunga mabao mawili Nou Camp bila
kufungwa bao jingine ndipo angalau wajipe matumaini ya kusonga.
Wenger ansema Arsenal watahitaji kushambulia sana
Beki wa Arsenal Laurent Koscielny atarejea kuwaongeza nguvu
baada ya kukaa nje kutokana na jeraha.
"Tumeshinda katika kila uwanja Ulaya lakini huko (Nou
Camp) hatujafanikiwa bado,” anasema Wenger.
"Mtazamo wetu haukuwa mbaya lakini tuliteleza na
tukaadhibiwa.
"Itatupa moyo sana kipindi kilichosalia cha msimu iwapo
tutacheza vyema Jumatano.
"Huwa twapigana kushinda vikombe na kwa sasa hatupigiwi
upatu kushinda msimu huu. Lakini bila kujali changamoto, Ligi ya Premia bado
iko wazi na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya nafasi ni finyu sana.”
Messi ndiye aliyefungia Barca mabao mechi ya kwanza
Barcelona, chini ya mkufunzi wao Luis Enrique, wamo alama
nane mbele La Liga na wanapigania kuwa klabu ya kwanza kuhifadhi Ligi ya Klabu Bingwa
Ulaya tangu kubadilishwa jina kutoka Kombe la Ulaya 1992.
Mechi itaanza saa 22:45 saa za Afrika Mashariki.
Mechi nyingine ya hatua ya 16 bora inayochezwa leo ni kati ya
Juventus na Bayern Munich.
BBC
No comments:
Post a Comment