Tanzania imeendelea kutamalaki kimataifa baada ya mwakilishi wake mwingine kuibuka kidedea ugenini, Azam FC imepata ushindi wa bao 3-0 dhidi ya wapinzani wao Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kombe la shirikisho ikiwa ni saa chache baada ya Yanga kupata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya APR Kigali, Rwanda.
Azam walipata bao la kwanza lilifungwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 50 baada ya kuachia shuti kali nje ya 18 kufuatia kona iliyopigwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ kuokolewa vibaya na mabeki wa Wits kisha mpira kumkuta Sure Boy.
Dakika ya 57 baadaye, beki wa pembeni wa Azam FC Shomari Kapombe aliipatia Azam bao la pili baada ya mabeki wa Wits kufanya uzembe kuokoa mpira kisha Kapombe akaserereka na kupiga mpira uliotinga moja kwa moja kwenye kamba za Wits.
John Bocco ‘Adebayor’ alihitimisha kipigo hicho kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 60 na kuiweka Azam kwenye mazingira ya kusonga mbele mbele kwenye michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment