Timu ya Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR FC ya Rwanda kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya klabu bingwa Afrika mchezo ukipigwa kwenye uwanja wa Amahoro, Rwanda.
Juma Abdul alizitoboa nyavu za APR kwa shuti kali kuiandikia Yanga bao la kwanza dakika ya 20 kwa mpira wa adhabu ndogo kufuatia Donald Ngoma kuangushwa na beki wa APR Rwatubyaye mita 10 kutoka kwenye box la penati.
Dakika ya 75 Thaban Kamusoko akafunga bao la pili akilitendea haki pande la Donald Ngoma kisha kupiga shuti akiwa ndani ya box na kuifungia Yanga bao la pili.
Wakati mchezo unakaribia kumalizika, APR walipata goli la kwanza kutokana na makosa ya golikipa wa Yanga Ally Mustafa ambaye aliutema mpira kwenye miguu ya Patrick Sibomana ambaye alifunga goli hilo dakika ya 90+3.
Yanga itakuwa nyumbani kuikaribisha APR FC kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa March 19, 2016 kwenye uwanja wa taifa, Dar es Salaam.
Takwimu muhimu
- Yanga imekutana na APR FC kwa mara ya tatu kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika. Mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo, Yanga ilikubali kichapo cha bao 1-0 lakini leo Yanga imeshinda kwa bao 2-1.
- Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite walikuwa wanacheza dhidi ya timu yao waliyowahi kuitumikia miaka kadhaa iliyopita.
- Kikosi cha APR kilichocheza dhidi ya Yanga kilikuwa na wachezaji wazawa kwa 100% wakati Yanga walikuwa na wachezaji mchanganyiko, wachezaji wazawa na wale wa kigeni.
No comments:
Post a Comment