Kamati ya Uchaguzi ya chama cha soka Zanzibar (ZFA)
imetangaza rasmi tarehe ya kufanyika uchaguzi wa ZFA ambao unatarajiwa
kufanyika tarehe 14 mwezi ujao wa April.
Akizungumza na Mtandao huu katibu wa kamati hiyo Afaan Othman
alisema uchaguzi utafanyika kisiwani Pemba tarehe 14 April saa 4:00 asubuhi.
“ Tunategemea kufanya uchaguzi tarehe 14/04/2016 Kisiwani
Pemba, tunaweza kuufanya Gombani au kule Wesha Pwani”.
Aidha Affan amewataka wadau mbali mbali wa soka wajitokeze
kuchukua fomu za kugambania nafasi tatu zitakazogombaniwa katika uchaguzi huo
ambazo ni Urais wa ZFA, Makamu wa Urais ZFA Unguja na Makamu wa Urais ZFA Pemba
ambapo fomu za kugombania zitauzwa shs laki mbili.
“ Kwa wale wenye nia ya kuchukua fomu nawaomba wajitokeze kwa
wingi ili waje kuongoza soka la Zanzibar”.
Wakati huo huo kamati hiyo imezitaja Sifa 6 za kugombea
nafasi hizo tatu kwenye uchaguzi huo.
1. Mgombea awe Mzanzibari.
2. Mgombea awe na elimu kiwango cha kidato cha nne.
3. Mgombea awe na umri usiopungua miaka 30.
4. Mgombea awe na uzoefu wa kuongoza soka.
5. Mgombea asiwe mtu aliefungwa jela kwa kosa jinai.
6. Mgombea awe na akili timamu.
Pia kamati hiyo imetangaza siku za kuchukua fomu ambazo
zitaanza rasmi kuuzwa kesho tarehe 27/03/2016 na mwisho wa kuchukua fomu ni
tarehe 06/04/2016 ambapo pia tarehe 07/04/2016 itakuwa ni siku ya usaili.
Fomu za uchaguzi kwa upande wa kisiwa cha Unguja zitauzwa na
Suleiman Haji (Kibabu) ambae ni mwenyekiti wa kamati hiyo, na kule kisiwani
Pemba fomu zitauzwa na Affan Othman ambae ni Katibu wa kamati hiyo.
Kamati hiyo ina jumla ya wajumbe wa nne (4) ambao ni Khamis
Suleiman pamoja na Mmanga Mjaka wakiongozwa na Suleiman Haji (Kibabu) ambae ni
mwenyekiti na Affan Othman ambae ni Katibu wa kamati hiyo.
Katiba ya ZFA ya mwaka 2010 ndio itakayotumika katika zoezi
zima hilo la uchaguzi ambapo mtu yoyote atakaechukua fomu hatoredeshewa fedha
zake hata kama atajitoa kushiriki uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment