Tuesday 29 March 2016

CHUO/BASRA YAPUNGUZWA MATUMAINI PEMBA


Timu ya Mkungu Malofa jana iliizuia timu ya Chuo/Basra kukata tiketi ya kucheza ligi ya Zanzibar baada ya kuinyuka kwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi daraja la Kwanza taifa Pemba hatua ya 6 Bora ulipchezwa jana katika uwanja wa Gombani.

Katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi timu ya Chuo/Basra ingefanikiwa kushinda ingalikuwa ya kwanza kupanda daraja kwa kufikisha alama 9, na sasa itahitaji kushinda mchezo wake wa mwisho hapo kesho na timu ya Danger Boys.

Goli pekee la Mkungu Malofa lilifungwa katika dakika ya kwanza ya mchezo huo kupitia mchezaji wake Abdalla Moh`d (Mbongo).

Mchezo huo ambao ulichezeshwa na mwamuzi Faki Khatibu kutoka Wilaya ya Mkoani timu ya Chuo/Basra ilionyesha kutoridhika na baadhi ya maamuzi ya mwamuzi huyo jambo ambalo lilipelekea mashabiki wake kutoa maneno ya kashfa kwa mwamuzi huyo.

KWENGINEKO

Katika mchezo mwengine timu ya New Star iligawana alama 1-1 baada ya kutoka sare ya kufungana goli 1-1 katika mchezo uliochezwa wakati wa saa nane za mchana uwanjani hapo.

Leo kutakuwa na mchezo katika ya timu ya Wawi Star na Danger Boys katika uwanja wa Gombani wakati wa saa 10 jioni mchezo ambao unategemewa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji nafasi ya kuingia katika timu tatu zitakazopanda daraja.

Ligi hiyo hadi sasa inaongozwa na Wawi Star yenye alama 7 baada ya kucheza michezo mitatu, Chuo/Basra alama 6 imeshacheza michezo mine, Mkungu Malofa inashika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 5 na imeshacheza michezo mine.


Timu za Danger Boys, Maji maji na New Star zote zina alama 4 kila moja, hivyo kufanya hadi sasa timu zikibakiwa na mchezo mmoja mmoja kutokuwepo na timu iliyojihakikishia kupata nafasi ya kupanda daraja.

No comments: