Tangu soka
la Zanzibar kuwa na mashakani sasa linafika mwaka mmoja na miezi mitatu bado
viongozi wakuu wa chama hicho wanavutana na hii kupelekea kuzidi kuwaumiza
wadau wa soka Visiwani Zanzibar.
Ilianza kama
masihara mwishoni mwa mwaka 2014 Makamu Urais wa Unguja wa chama kinachosimamia
mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir (Mpakia) kwenda Mahakamani kufungua
Kesi nambari 62 ya mwaka 2014 dhidi ya viongozi wenzake wakuu wa ZFA Ravia
Idarus Faina (Rais ZFA), Kassim Haji Salum (Katibu ZFA) na Ali Mohammed (Makamo
rais ZFA Pemba).
Jambo hilo
limepelekea soka la Zanzibar kuathirika sana kwa sekta tofauti ambapo miongoni
mwa athari zilizoikumba ni kuchezwa ligi pasipo na udhamini wowote ambapo kila
mdhamini ambao awali walionesha nia ya kudhamini ligi hiyo walikimbia upesi
wasije kupata aibu kwa ligi ambayo wanaidhamini wao ina mushkeli.
Awali Ligi
kuu ya Zanzibar ilikuwa iyanze tangu tarehe 15/9/2015 lakini ilisimamishwa na
mahakama kufutia timu ya Chuoni na Aluta kuifungulia kesi ZFA, jambo ambalo
lililopelekea mpaka ligi hiyo kucherewa kuanza na ilianza Mwezi Novemba mwaka
Jana (2015).
Rundo la
timu kupandishwa kiholelea lilijitokeza ambapo msimu ulopita wa mwaka 2014-2015
ligi kuu soka Zanzibar ilikuwa inatimu 12 tu, lakini msimu huu ni vichekesho
timu 29 ligi hiyo imejumuisha, timu 15 za Unguja na timu 14 za Pemba ambapo
kuna timu zilitoka ligi daraja la pili taifa hadi ligi kuu pasipo hata kupita
ligi daraja la kwanza taifa.
Jambo hilo
likapelekea ligi kuchezwa viwanja ambavyo havina hadhi ya kuchezwa ligi kuu ya
nchi, uwanja wa Bweleo na uwanja wa Wimbi Ndijani, ambapo wadau wengi wa soka
wakaanza kuita ligi hiyo majina tofauti, mara Kipwida na wengine waliita
Bonanza tu na sio ligi.
Athari
nyengine iliojitokeza ligi inachezwa lakini kwa kanda moja tu ya Unguja ambapo
ni ligi kuu ya Zanzibar lazima ichezwe kanda zote mbili yani kanda ya Unguja na
Pemba, lakini pia kati ya timu 15 za Unguja, tmu 14 zilikubali kucheza ligi
isipokuwa timu moja tu ya Malindi kususia kucheza ligi hiyo kwa kutoitambua
kamati ya muda iliongoza ligi hiyo.
Soka la
Zanzibar kwa kipindi likawa lipo Mahakamani jambo ambalo vilabu vya Zanzibar
vilipata hasara kubwa kuhudumia timu zao pasipo hata kuchezwa ligi, na
wachezaji walivunda maana walifanya mazoezi kusubiri ligi mpaka wengine
walishindwa na kupelekea hata vifaa vyao vya michezo kufanyia shughuli
nyengine.
Tarehe
2/9/2015 Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ilisimamisha kozi zao zote
kufanyika Zanzibar zikiwemo hata kozi za Makocha ambapo ilikuwa tayari
ishaandaliwa Kozi ya makocha ya leseni B iliokuwa ifanyike kuanzia tarehe
5/9/2015 ambapo CAF iliitumia barua ZFA kuwa kozi hiyo wameizuia kutokana na
soka la Zanzibar kuwepo Mahakamani.
ZFA
iliathirika sana mana Mkufunzi wa kuendesha kozi hiyo Sunday Kayun alikuwa
tayari kashakatiwa tiketi ya Ndege kwa ajili ya kuja kuwanowa makocha Visiwani
Makocha
wengi walipata hasara kwa hilo maana walikuwa wanatarajiwa kushiriki katika
kozi hiyo ni makocha wa Zanzibar, Tanzania bara na mmoja kutoka Zambia, ambao
ni Ibrahimm Mohd Makeresa, Omar Khamis Othman, Abubakar Issa Simai, Ali
Suleiman Haji, Mohd Abass Silima, Ramadhan Abdulrahman, Yussuf Ramadhan, Sheha
Khamis Rashid, Salim Haji Mwadini, Iddi Mohd Ali, Ali Abdallah Hassan, Juma
Awadh Khatib, Juma Yussuf Sumbu, Mzee Ali Abdallah, Hafidh Muhidin Mcha, Mussa
Hassan Jaribu, Asaa Khamis Mtwana, Hamad Mzee Shilingi, Jumanne Chalse, Mbwana
Mtem, Renatus Shija, Tegete, Mrage Kabange, Ali Mohd Ameir, Seif Bausi, Bakar
Ali Hamad, Saleh Alawi Abdallah, Suleiman Mahmoud, Masoud Salum Abdi na wa
mwisho ni David Solopi ni kutoka Zambia.
Jumla ya
makocha wote hao wamekosa fursa ya kozi hiyo, pengine wakizidi kusaidia soka la
Zanzibar baada ya kupatiwa mafunzo hayo.
Hilo ni soka
la Zanzibar ambalo limechafua kila sehemu kwasasa, wawakilishi wa Zanzibar
katika michuano ya Kimataifa ya klabu bingwa na kombe la shirikisho timu ya
Mafunzo na JKU nao waliathirika na hilo la Soka kuwepo Mahakamani maana hata
maandalizi yao yalikuwa ni ya kusuwa suwa, mara wanaambiwa hamtoshiriki, mara
mtashiriki, hili pia limewatoa mchezoni wachezaji wa timu hizo japo kuwa JKU
amesonga hatua nyengine ya kombe la Shirikisho kufuatia wapinzani wao timu ya
Gabarone United ya Bostwana kujitoa katika mashindano hayo.
Hii
inaonesha hata Mafunzo ambae ni bingwa mtetezi wa ligi kuu soka Zanzibar
angeweza kufanya vizuri au hata kupunguza idadi ya mabao katika michuano ya
klabu bingwa barani Afrika alipotolewa na AS Vita Club ya DR Congo ambapo jumla
kafungwa mabao 4-0 kufuatia 0-3 alizofungwa nyumbani kwao Zanzibar na 1-0
alilifungwa huko DR Congo jumapili ilopita.
Jumamosi ya
tarehe 27/2/2016 ZFA walifanya Mkutano mkuu wa dharura wa ZFA TAIFA ambapo
wajumbe waliamua maamuzi mazito katika mkutano huo.
Ajenda tatu
zilijadiliwa katika mkutano huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Wizara ya
Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Kikwajuni Mjini Unguja ambapo miongoni mwa
mada tatu zilizojadiliwa, moja ni kujadili mwenendo wa kamati tendaji ambapo
muwasilishaji wa mada hiyo alikuwa Makamu wa Urais ZFA Unguja Haji Ameir
(Mpakia) ambae hakuonekanwa katika mkutano huo na mada yake hiyo ikawasilishwa
na Makamu wa Urais ZFA Pemba Ali Mohammed.
Baada ya
kusikiliza mada hiyo wajumbe 50 waliokuwepo kwenye ukumbi huo wamekubaliana
kupiga kura, kura ambayo ilikuwa inamuhusu Makamu wa Urais Unguja Haji Ameir
aliepeleka kesi ya soka Mahakamani mwishoni mwa mwaka 2014 ambapo wajumbe
walitaka afukuzwe kwenye chama hicho na asijihusishe na mambo ya michezo kwa
muda wa miaka 4.
Wajumbe 50
wakapiga kura ambapo wajumbe 43 walisema afukuzwe na wajumbe 4 walisema
asifukuzwe ambapo wajumbe 3 hawajapiga kura.
Hivyo Alhaj
Haji Ameir ambae ni Makamu wa Urais ZFA Unguja alifutwa rasmi nafasi hiyo na
kutojishughulisha na mambo ya michezo kwa muda wa miaka 4.
Aidha
mkutano huo uliiyondoa kamati ya muda iliokuwa ikiongoza soka la Zanzibar
ambapo wajumbe 42 walisema kuwa kamati hiyo iondoke na wajumbe 6 walisema
wasiondoke wakati wajumbe 2 kati ya hao 50 hawajapiga kura.
Ajenda ya
pili iliyowasilishwa katika mkutano huo kuhusu kuteuliwa Mkaguzi wa Mahesabu
yaani 'Auditors' kwa ajili ya kuvipitia vitabu vya mahesabu vya Chama hicho
ambapo mkutano huo umekubaliana kuchaguwa Kampuni yenye sifa kufanya ukaguzi wa
Mahesabu kwa ZFA Taifa ambapo utafanyiwa tangu uongozi wa ZFA wa mwaka 2012
hadi 2016, yani kipindi cha Rais Amani Makungu na Ravia Idarous Faina wa sasa.
Na ajenda ya
tatu mkutano mkuu ulikuwa unatakiwa kuamua kuteuwa wajumbe 5 watakaoandika upya
Katiba ya ZFA ambapo wajumbe 5 walioteuliwa kati ya hao 12 waliopendekezwa
Awali ni Eliud Peter Mvella kura 46 (Msaidizi mkurugenzi TFF na Mwanasheria),
Saleh A. Said kura 43 (Wakili upande wa ZFA), Affan Othman Juma kura 42 (Kiongozi
wa mpira na taaluma ya sheria) Ame Abdalla Dunia kura 40 (Mwalimu/Taaluma ya
Sheria), na Othman Ali Hamad kura 36 (Mwanasheria, Kiongozi na mchezaji wa
mpira).
Aidha
mkutano huo umehalalisha wajumbe waliokuwepo kwenye ZFA Wilaya ya Magharibi “B”
kuwa ni halali na wanatambuliwa na mkutano mkuu na hautofanyika tena uchaguzi
kwenye Wilaya hiyo.
Kuhusu
uchaguzi wa ZFA Taifa mkutano huo umetowa tarehe ya kufanyika Uchaguzi huo
ambao unatarajiwa kufanyika April 9, 2016 huko Kisiwani Pemba ambapo nafasi ya
Urais, Makamu Urais Pemba na Makamu Urais Unguja ndizo nafasi tatu
zitagombaniwa katika uchaguzi huo ambapo pia katiba itakayotumika ni ya mwaka
2010.
Jambo
jengine katika mkutano huo ni Ligi kuu soka Zanzibar kanda ya Unguja ambayo
imeendeshwa na Kamati ya Mpito iliofutwa leo hii, kwa makubaliano ya mkutano
huo ligi hiyo wamesema ni halali na wanaikubali, na ligi kanda ya Pemba
karibuni itaanza kuchezwa baada ya kukaa kamati tendaji.
Lakini baada
ya kufutwa Makamu Urais ZFA Unguja Haji Ameir (Mpakia) yeye alisema kuwa ni
ukiukwaji wa katiba na sheria walichofanya wenzake kumuondosha katika chama
hicho na kusema kuwa hawana uwezo wa kumfukuza na yeye atarudi tena Mahakamani.
Soka la
Zanzibar linazidi kusikitisha kitu si kitu Mahakamani na hili wadau wengi wa
soka ambao hawajapenda majina yao kuandikwa humu walisema kuwa viongozi wote
wanaongoza ZFA hawafai na waondoshwe wote ili soka linusurike.
“ ZFA nzima
haifai na wao ndio wanatuharibia mpira wetu, ili soka letu lirudi hadhi yake
kama ya zamani, basi viongozi wote wa ZFA hawafai waondoke, wanatuumiza ,
hatuwataki, kila siku Mahakamani ndo nini!, Mpakia, Ravia na Ali Mohammed wote
hawafai, wajiuzulu tumewachoka, sisi tunajua pale ZFA pana rundo la pesa ndo
mana hawataki kuondoka, na sijui kama hawatorogana, hatuwataki watuachie mpira
wetu kwasababu tunaongozwa na watu ambao si wa Mpira”. Walisema Wadau.
Hilo ndio
soka la Zanzibar bado halijakaa sawa sawa mpaka leo tangu mwaka 2014
lilipokwenda Mahakamani ambapo kwasasa kesi hizo zimeshafutwa.
No comments:
Post a Comment