Timu ya Judo Zanzibar
imerejea visiwani wakitokea Bunjumbura Burundi wakishinda nafasi ya pili katika
mashindano ya kumi ya Afrika Mashariki yaliofanyika huko.
Zanzibar wameshinda nafasi
ya pili katika mashindano hayo ambapo wamefanikiwa kuibuka na Medali za dhahabu
2, fedha 1 na shaba 2.
Walioshinda Medali hizo
kwa Zanzibar ni Hafidh Makame alishiriki Judo chini ya kilo 73 ambapo alishinda
Dhahabu, na Masoud Kombo pia ameshinda Dhahabu akishiriki Judo chini ya kilo
100.
Wengine walioshinda medali
wakitokea Zanzibar ni Mohammed Abdul rahman akishinda medali ya Fedha ambapo
kashiriki judo ya juu ya kilo 100 na Abdul rabi Alawi yeye ameshinda fedha judo
chini ya kilo 66.
Na mwana mama pekee
aliotokea Zanzibar katika mashindano hayo Salma Omar amerudi na medali ya shaba
akishinda chini ya kilo 52.
Burundi waliongoza katika
Mashindano hayo ambapo walishinda medali za dhahabu 3, fedha 5 na shaba 3.
Yussuf Thabit Mbalambula
ambae ni meneja katika msafara wa timu hiyo ya Zanzibar alisema kuwa mashindano
yalikuwa magumu sana na pia wanashukuru wamerudi salama Zanzibar.
“Ukweli mashindano
yalikuwa magumu sana, lakini vijana wangu wamepigana na tumefanikiwa kushinda
nafasi ya pili, pia tunawashukuru sana wenyeji wetu Burundi walitupatia ulinzi
mkubwa sana, maana hatari sana kulikuwa kule, lakini tulilindwa sana
tunawashukuru Balozi wetu wa Tanzania nchini Burundi katupa ushirikiano mkubwa
sana”. Alisema Thabit.
Katika mashindano hayo
yalijumuisha nchi 4, wenyeji Burundi ambao walishinda nafasi ya kwanza,
Zanzibar nafasi ya pili, nafasi ya tatu ilishikwa na Kenya na mwisho ilikamatwa
na Ethiopia ambapo jumla ya washiriki wote ni 62 katika mashindano hayo ambapo
wenyeji Burundi walishiriki 33, Zanzibar 8, Kenya 20 na Ethiopia mshiriki 1
pekee.
No comments:
Post a Comment