Wednesday 6 April 2016

Higuain afungiwa mechi 4 kwa kumkemea refa


Mshambuliaji wa Napoli apewa adhabu kwa kumkosea heshima refa kwenye mechi ya Serie A

Nyota wa Argentina anayechezea kilabu ya Napoli nchini Italia Gonzalo Higuain, amefungiwa mechi 4 kutokana na utovu wa nidhamu uwanjani.

Higuain alipewa adhabu hiyo na kamati ya nidhamu ya soka nchini Italia baada ya kumkosea heshima refa wakati wa mechi ya Serie A iliyochezwa kati ya Napoli na Udinese.

Katika mechi hiyo, Higuain alionyeshwa kadi nyekundu inayojumuisha njano ya pili dakika ya 75 na kulazimika kuiacha Napoli kumaliza mechi hiyo na wachezaji 10.

Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa refa Massimiliano Irrati, Higuain aliamua kumkemea na kuzusha rabsha kabla ya kutoka.

Napoli iliyokuwa ikicheza ugenini ilishindwa na Udinese mechi hiyo 3-1.

No comments: